Loading...

Mawakili 30 matatani kwa kukiuka maadili

Mawakili 30 wameshtakiwa kwenye Kamati ya Mawakili wakidaiwa kukiuka miiko ya taaluma yao ikiwamo kung’angania majalada ya kesi na kuwasababishia usumbufu wateja wao.


Akizungumza juzi kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti mawakili wapya 624, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande alisema kwa kawaida jalada ni mali ya mteja, lakini baadhi ya mawakili hugoma kuyakabidhi kwao wanapoamua kuhamishia kesi zao kwa wakili mwingine.


“Kazi hii nayo ina miiko yake, natoa wito kwa mawakili wapya wote kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa kazi zao na kuwa waaminifu kwa wateja wao na jamii kwa ujumla, huku wakitambua kwamba wao ndiyo msingi wa haki kupatikana kwa mujibu wa sheria,” alisema Jaji Chande.


Alisema ongezeko la idadi ya mawakili waliofuzu inaongeza idadi yao nchini inayofikia 6,424 na inaongeza wigo wa huduma ya kisheria kupatikana kwa wananchi waishio katika maeneo tofauti nchini. “Hata hivyo, kwa idadi hiyo bado hatujajitosheleza tukilinganisha na idadi ya Kenya ambao wana mawakili zaidi ya 14,000 na Uganda 2,500, tunatumaini kwamba wataongeza uwajibikaji kulingana na taaluma yao na watazingatia maadili,” alisema.


Wakili Frank Ntabaye ni miongoni mwa waliotunukiwa vyeti, alisema amejiandaa kuwatumikia wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria, hasa katika kesi zinazohusu migogoro ya ardhi na mirathi.


“Natambua kuna watu wanaonewa wanakosa haki zao kutokana na kutojua sheria, sasa kuanzia leo nami nikiwa nimeongeza idadi ya mawakili nchini, nitashiriki kikamilifu kutoa msaada wa kisheria kwa wale wanaohitaji wakiwamo wasio na uwezo wa kifedha,” alisema Wakili Ntabaye.


Wakili mwingine, Happiness Mehena alisema amekusudia kujikita kuwasaidia watu wenye migogoro ya kifamilia na watoto wanaonyanyaswa kwa kufanyiwa vitendo vya kikatili.


Kwa upande wake, Wakili Idd Yassin alisema amejiandaa kuwa wakili wa kujitegemea ili aweze kuwa na nafasi nzuri ya kujituma katika kusaidia watu wanyonge kupitia mahakama, wapate haki zao.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHACHANDU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top