Akizungumza na waandishi wa habari jana Ulrich Matei, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amesema kuwa, askari huyo ‘feki’ ambaye hakuwa na cheo (private), alikamatwa Julai 13 mwaka huu saa 10 jioni ndani ya Kituo cha Mabasi Msamvu wakati akielekea Dumila wilayani Kilosa.Kamanda Matei amesema kuwa, askri huyo feki alikamatwa wakati akitokea Dar es Salaam na alipofika Msamvu, alishuka kwa lengo la kutafuta maji ya kunywa ndipo askari polisi waliokuwa doria katika kituo hicho walipomtilia shaka na kumkamata.
Akihojiwa na askari mara baada ya kukamatwa alidai kuwa, sare hizo ni za ndugu yake ambaye ni askari wa JWTZ Kikosi cha Malamba jijini Tanga na kwamba, alivaa sare hizo ili kukwepa kulipa nauli kwenye basi alilokuwa akisafiria.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuvaa hizi sare, kaka yangu ndio askari na alipokuja nyumbani Dar es Salaam ndipo alipoziacha hizi sare hivyo mimi niliona nizivae ili nisilipe nauli kwenye basi wakati nakwenda Dumila kwa kaka yangu mwingine kuchukua fedha za matumizi,” amesema.
Aidha mtuhumiwa huyo amedai kuwa, kazi yake ni mfanyabiashara wa mitumba jijini Dar es Salaam.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye ndugu askari kutojaribu kuvaa sare za jeshi lolote kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na watachukuliwa hatua.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakama mara baada ya kuhojiwa na upelelezi kukamilika ikiwa ni pamoja na kumtafuta ndugu yake ambaye ni askari mwenye sare hizo.
Post a Comment