BILIONEA Mtanzania, Said Salim Bakhresa, amepanga kutumia dola za Marekani milioni 30 sawa na Sh bilioni 65.5 kuchukua umiliki wa kiwanda cha usagishaji Zimbabwe, Blue Ribbon Industries (BRI).
Kwa mujibu wa gazeti la Zimbabwe Mail, Bakhresa Group, moja ya himaya kubwa ya kampuni nchini Tanzania, imeifahamisha rasmi Tume ya Ushindani na Forodha ya Zimbabwe kuwa inapanga kununua umiliki wa asilimia 100 wa kampuni hiyo iliyotaabani.
Mwaka 2014, Bakhresa Group ilishinda zabuni ya kumiliki hisa katika BRI baada ya wanahisa wake wakuu kukaribisha zabuni kwa wawekezaji wainunue au kuingiza mtaji katika BRI ili kufufua operesheni za kampuni hiyo.
BRI, ambao ni watengenezaji wa mkate na vyakula vya mifugo imekumbwa na matatizo ya kifedha na ilikuwa ikihangaika kulipa mikopo iliyokopa kutoka ubia wa mabenki ya Zimbabwe na washirika wa kibiashara.
Bakhresa, ambayo ni kampuni inayoongoza kwa shughuli za usagishaji nchini Tanzania, ikiendesha shughuli katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki, imeonesha kuwa inatarajia kuwekeza mtaji huo wa Sh bilioni 65.5 kwa BRI na kuirudisha kampuni katika shughuli za uingizaji faida.
Lakini mpango huo ulikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa washindani na Tume ya Ushindani na Forodha ya Zimbabwe imekuwa ikisuasua kuipitisha.
Said Salim Bakhresa, ambaye ni mwasisi wa Bakhresa Group, anashika namba tatu kwa utajiri Tanzania, kwa mujibu wa Forbes wenye thamani ya dola milioni 600.
Kampuni yake hiyo inajihusisha na biashara ya kilimo, vinywaji, vyombo vya habari, lojistiki, biashara ya mafuta, utengenezaji bidhaa na ufungashaji.
Post a Comment