Loading...

Mbwembwe za Madereva Barabarani zaua Mume, Mke na Mtoto

Ni kawaida kwa madereva wa mabasi ya kampuni moja kufanya mbwembwe wakati wanapokutana njiani kutoka mikoa tofauti, lakini za madereva wa City Boys hazikuwa kwenye mahesabu mazuri.

Wako madereva wanaosimama kuzungumza kwa muda na baadaye kila mmoja kuendelea na safari yake, na wengine wanaosalimiana kwa kuwasha taa bila ya kupunguza mwendo.

Lakini mbwembwe za madereva wawili wa mabasi ya kampuni ya City Boys, ni za hatari; wanapokutana njiani hutoka upande ambao hutakiwa kuutumia na wote kuwa upande mmoja kabla ya kila mmoja kurejea upande wake kuendelea na safari.

Kibaya zaidi hawapunguzi mwendo ili kuweka tahadhari ya ajali.
Ndivyo ilivyokuwa juzi wakati mabasi ya City Boys yalipogongana kwenye Kijiji cha Maweni mkoani Singida na kuua watu 31, ikiwamo familia ya mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mvomero, Morogoro ambaye alikuwa akitokea mkoani Tabora kujitambulisha akiwa na mchumba na watoto wake.

Kutokana na mbwembwe hizo, Jeshi la Polisi linataka kuwashtaki madereva hao kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia.

Ajali hiyo iliyosababisha watu 54 kujeruhiwa ilitokea saa 8.15 mchana Tarafa ya Kitinku mkoani Singida.

Kamanda wa polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema moja ya mabasi hayo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Kahama na jingine likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam.

Kamanda Mpinga alisema kuwa sababu za kutokea kwa ajali hiyo ni utani wa madereva kusalimiana kwa kufuatana upande mmoja na kuwashiana taa kabla ya kupishana njiani.

“Mmoja wa madereva alishindwa kurudi katika upande wake na kusababisha mabasi hayo kugongana uso kwa uso kutokana na mwendo kasi,” alisema Kamanda Mpinga.

“Hii ajali iliyotokea jana (juzi) si ya kawaida. Madereva wote wawili tutawashtaki kwa kosa la kufanya mauaji bila kukusudia kutokana na chanzo cha ajali hii.”

Aliongeza kuwa madereva wengi wamekuwa wakikiuka sheria inayowataka kuendesha kwa kasi ya kilomita 80 kwa saa, akisema waliwahi kukamata basi moja kati ya yaliyopata ajali ambalo lilikuwa likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam likiwa kwenye mwendo wa kasi ya kilomita 122 kwa saa. Basi hilo lilikamatiwa Singida Mjini na kuandikiwa faini ya Sh30,000.

Kamanda wa polisi wa Singida, Thobias Sedoyeka pia alizungumzia mbwembwe za madereva hao kuwa ni mambo yaliyochangia ajali hiyo.

“Inaelekea hawa madereva wanaelewana au ni marafiki wa karibu kwa kuwa walipokaribiana, waliwashiana taa ikiwa ni ishara ya kusalimiana,” alisema Kamanda Sedoyeka.

“Baada ya hapo, kila moja alihama upande halali alikokuwa na kuhamia upande mwingine na mwenzake naye alitaka kufanya hivyo. Lakini kutokana na mabasi hayo kuwa mwendo kasi, mahesabu yaliwashinda na kusababisha yagongane.”

Abiria wa basi lililokuwa likitokea Kahama, Ibrahimu Samwel alisema basi likiwa kwenye mwendo wa kasi, ghafla alisikia kishindo kikubwa na kisha lilipinduka na kusababisha taharuki kubwa kwa abiria.

Familia ilivyomalizwa ajalini
Ajali hiyo ilichukua maisha ya mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mvomero, Peter Pinto aliyekuwa akitokea Tabora kumtambulisha mkewe kwa wazazi wake baada ya kufunga ndoa mkoani Mbeya.

Akizungumza jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako baadhi ya majeruhi na maiti walipelekwa, Said Mussa, ambaye ni ndugu wa mwalimu aliyefariki kwenye ajali hiyo, alisema katika ajali hiyo amepoteza baba yake mdogo, mke wa baba mdogo wake na mtoto mdogo.

Alisema Pinto, ambaye ni baba yake mdogo, alikuwa ametoka kumtambulisha mkewe kwa wakwe zake.

“Walifunga harusi mkoani Mbeya ukweni kwa hiyo walikuwa wakitoka kutambulisha nyumbani kwa baba mdogo mkoani Tabora,” alisema.

Mtoto wa dada wa marehemu, Stephano Antony alisema marehemu Pinto (32) alifunga ndoa miaka mitatu iliyopita na Joyce William (26) katika Kanisa la Mashahidi ya Jehova lililoko Mbalali mkoani mbeya.

Alisema katika ndoa yao walifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike anayeitwa Neema Peter mwenye umri wa miaka miwili na nusu.

Alisema Joyce ni mama wa nyumbani aliyekuwa na mpango  wa kujiendeleza.
Alisema kuwa wote watatu watazikwa Urambo baada ya ndugu wa marehemu anayeitwa Joyce kuwasili.

Majeruhi walicheleweshwa
Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ibehzi Ernest alisema changamoto waliyoipata kutokana na ajali hiyo ni kucheleweshwa kwa majeruhi.

“Madaktari na wauguzi walikuwa wamejipanga kuhudumia majeruhi, lakini walifikishwa hapa saa 6.00 usiku wakati miili ya watu waliofariki dunia ilifikishwa saa 11:00 jioni,” alisema.

Dk Ernest alisema kati ya majeruhi 15, mmoja alifariki saa 3.00 asubuhi jana asubuhi na hivyo kufanya idadi waliofariki dunia kufikia 31.

Alisema watu 13 waliofariki dunia hadi jana mchana walikuwa wametambuliwa na ndugu zao, akiwamo Ismail Bashe, ambaye ni ndugu wa mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).

Hata hivyo, alisema miili ya watu waliofariki dunia ilikuwa katika hali mbaya ikiwa ni pamoja na kukatika vichwa na sehemu nyingine ubongo kuonekana chini bila kiwiliwili.

Alisema mmoja wa majeruhi, Katra Abubakary ndiye aliyelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

“Kati ya majeruhi 15, watano walikuwa wamevunjika miguu na mikono na hivyo kutokwa damu nyingi. Walifanyiwa upasuaji usiku wa kuamkia jana.”

Kamanda wa Polisi wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema jana dereva wa basi lililokuwa likitokea Dar es Salaam, Jeremia Maritin (34) ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam anashikiliwa na polisi.

Kamanda Sedoyeka alitoa wito kwa ndugu na jamaa ambao ndugu zao walisafiri na mabasi hayo, kufika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na ya Mkoa wa Dodoma ili kutambua miili ya ndugu zao.

“Majeruhi wengi wamevunjika miguu, mikono na wengine sehemu mbalimbali za miili yao. Baadhi ya majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na hali zao zinaendelea vizuri.”

Meneja wa Tanroads wa Singida, Leonard Kapongo alisema katika eneo hilo, hakujawahi kutokea kwa ajali za magari.

“Kwa uzoefu wangu wa muda mrefu, eneo lenye ajali za mara kwa mara za magari ni Mlima Saranda kutokana na ukali wa kupanda na mteremko mkali. Hii ajali mbaya ya juzi siri yake wanaijua vizuri madereva wa mabasi hayo,” alisema.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHACHANDU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top