SERIKALI iliyoundwa na Dk. Ali Mohamed Shein baada ya kufutwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa 25 Oktoba 2015 imesema, pendekezo la kuwepo serikali ya mpito ni ‘upuuzi mtupu’, anaandika Mwandishi Wetu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Balozi seif Ali iddi katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) uliojadili na kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Balozi Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema, hakutakuwa na serikali ya mpito wala ya mseto pia hakutakuwa na uchaguzi mwingine kabla ya mwaka 2020.
Kauli ya Balozi Seif inatokana na malalamiko ya Chama cha Wananchi (CUF) kutaka kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa maeleza kuwa, Dk.Shein amerejea madarakani kwa njia haramu.
Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea urais wa CUF visiwani anaelezwa kushinda.
Kabla ya kumalizwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo kwenye majimbo yote Zanzibar, Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) alifuta matokeo ya uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa kasoro mbalimbali.
Hatua hiyo ililalamikiwa na kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, wasomi, makundi ya kutetea haki pamoja na mataifa ya nje.
Pamoja na malalamiko hayo, ZEC chini ya Jecha ilitangaza marudio ya uchaguzi kuwa tarehe 20 Machi mwaka huu kinyume na Katiba ya Zanzibar.
Hatua hiyo ilisababisha CUF na vyama vingine vha upinzani kugomea marudio ya uchaguzi hu.
Hali hiyo iliiweka Zanzibar katika sintofahamu na hata kusababisha majeshi ya nchi kuelekezwa visiwani humo huku baadhi ya raia wakitajwa kukimbia kisiwa hicho kuhofia kutokea machafuko kama ilivyokuwa mwishoni mwaka 2000.
Post a Comment