Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe ameagiza wenyeviti wa halmashauri 18 nchini
zinazoongozwa na Ukawa kuacha utaratibu wa kutoa fedha za halmashauri
kuwasaidia mafuta ya magari wakuu wa wilaya au kuzitumia kwa ajili ya
masuala ya kisiasa ya vyama vyao.
Akizungumza
na mameya na wenyeviti wa halmashauri zinazoongozwa na Ukawa katika
mkutano uliofanyika juzi mjini Arusha, Mbowe alisema viongozi hao
wanapaswa kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa na halmashauri hizo
zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Alisema
katika kikao hicho cha mameya na wenyeviti wa halmashauri, wametambua
kuwa kuna matumizi mabaya ndani ya Serikali, mbali na wafanyakazi hewa
ambao wapinzani wamekuwa wakilalamika tangu mwaka 2005.
Mbowe
alisema bado kuna halmashauri ambazo zimekuwa zikitumia fedha kufadhili
ofisi za wakuu wa wilaya na chama tawala, jambo ambalo sasa kwa
halmashauri za Ukawa halitakuwapo.
“Maeneo
ambayo wakuu wa wilaya wamezoea kuomba fedha za mafuta na CCM wamekuwa
wakiomba fedha kwa ajili ya kazi zao tunawaambia wasithubutu tena kwenda
kwenye halmashauri zinazoongozwa na Ukawa, kwani hatutawapa fedha na
tunawaumbua,” alisema.
Mbowe
alisema katika halmashauri za Ukawa hawataki kusikia kuna fedha
zimetolewa kwa wakuu wa wilaya au chama chochote cha siasa.
Alisema
katika kikao hicho wamekubaliana kuanzisha mipango mikakati ambayo
itawezesha kubuniwa vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni rafiki kwa
wananchi, kupatikana kwa ajira na kuboresha huduma muhimu za Watanzania.
Akizungumza
baada ya maelekezo hayo, Mwenyekiti wa Madiwani Chadema nchini ambaye
pia ni Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema watatekeleza na
hawatakubali kuingiliwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na makatibu
tawala.
Calist
alisema katika halmashauri za Ukawa uamuzi wa mwisho wa uendeshaji wa
halmashauri utafanywa na madiwani na siyo mtu kutoka nje ya halmashauri
hizo.
“Tutasimama na kutetea mamlaka ya kisheria ya Serikali za mitaa hapa nchini,” alisema.
Katibu
wa Madiwani wa Ukawa nchi nzima ambaye ni Meya wa Kinondoni, Boniface
Jacob alisema watahakikisha wanasimamia utendaji mzuri wa halmashauri
zote wanazoziongoza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Post a Comment