Ukosoaji huo unakuja baada ya baadhi ya majina ya walioteuliwa katika nafasi hizo kuonekana zaidi ya mara moja katika nafasi mbili tofauti, hatua inayotajwa kuashiria kutokuwepo kwa umakini wakati wa uandaaji wa orodha ya majina hayo au uteuzi huo.“Inashangaza! ofisi ya rais ina watumishi wangapi hata kushindwa kuhakiki majina 200?
Kama ofisi kubwa kiasi hicho inashindwa kuhakiki wateuzi hao, je nchi inawezaje kuhakiki maelfu ya watumishi wa serikali yetu?” anahoji Eliud Ibrahim, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Ibrahim anasema, mara kadhaa Rais Magufuli na baadhi ya Mawaziri wamekuwa wakiwatia “tumbo joto” ama kuwafukuza baadhi ya watumishi wa serikali kuhusu usahihi wa taarifa wanazozitoa lakini wao wameonekana hawawezi kabisa.
“Tulishuhudia kutenguliw kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ana Kilango Malecela baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa jambo ambalo lilisababisha Ikulu kufanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza.
“Lakini pia tumeshuhudia zaidi ya mara moja Ikulu ikitoa taarifa kimakosa ikiwemo ile ya uteuzi wa Emile Ntakamulenga ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Serengeti lakini alipofika Ikulu wakati wa kuapishwa akaambiwa uteuzi wake ulikosewa. Nani anawajibika kwa uzembe huu?,” anasema Elizabeth Marunge., mkazi wa Dar es Salaam.
Miongoni mwa makosa yaliyofanywa na Ikulu jana ni uteuzi wa Dk. Leonard Massale ambaye alitangazwa jana kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma wakati tayari ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Post a Comment