Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango amesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa madai kwamba, mizigo kutoka nje ya nchi imepungua kutokana na ongezeko la kodi “kauli hii si ya kweli.”Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo katika mkutano wa uorodheshwaji wa hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mpango amefafanua kuwa, kuyumba kwa soko la China ndiyo sababu ya mizigo hiyo kupungua kwa kuwa, Tanzania inashirikiana na nchi hiyo katika masuala ya kiuchumi.
“Muangalie uchumi wa China unavyokwenda, soko lake limepungua ulimwenguni, kutokana na sababu ya nchi kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na china kumeathiri. Kodi haiathiri chochote kile, na kelele zote zinazoendelea zinafanywa na wale wakwepa kulipa kodi.
“Waambie waache porojo, waende kwenye takwimu, hata kwa nchi jirani ya Kenya mizigo inayoingia imepungua kwenye Bandari ya Mombasa. Waende wakapate ripoti.”
Amesema kuwa, serikali ipo makini na wafanyabishara ambao hawataki kulipa kodi. “Walipe kodi tu ili serikali iweze kuwahudumia, haiwezekani bandari itoe huduma kwa wafanyabiashara pasi na wao kulipa kodi, hapana.”
Kuhusu hisa 20,250,000 zilizoorodheshwa leo katika soko la hisa la Dar es Salaam Dk. Mpango amewataka wafanyabiashara wazawa kuitumia fursa hiyo kwa kununua hisa hizo ili kukuza mitaji yao.
“DSE iendeleze uboreshaji wa mfumo wa kiteknohama a soko ili kurahisisha ufikiwaji wa soko la hisa kwa watanzania waliopo nchini na wanaoishi nchi za nje.
“Na pia ningependa kuwahamasisha kuendelea kutumia ujio wa teknolojia mpya ya simu ya mkononi ili kufanikisha lengo hili,” amesema Dk Mpango.
Nasama Massinda, Kamishna wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) amesema, ongezeko la kampuni zinazowekeza kwenye DSE litaisadia serikali kupata mapato yake inavyostahili.
“Serikali itapata mapato yake inavyostahili kwa sababu ili wawekezaji waweze kuwekeza katika soko la hisa lazima mapato na soko lake liwekwe bayana na kwamba jambo hilo litaiwezesha serikali kutoza kodi inavyostahili,” amesema.
Kuorodheshwa kwa hisa 20,250,000 na DSE kunatokana na mauzo ya awali yaliyofanyika mnamo tarehe 16 Mei hadi Juni 3 mwaka huu ambayo yamewezesha upatikanaji wa fedha Sh. 10,125,000,000 na kwamba, kuorodheshwa huku ni muhimu kwa kuwa kutawezesha wawekezaji walionunua hisa katika soko la awali kupata fursa ya kuziuza na kuruhusu wawekezaji wapya.
Post a Comment