Loading...

Babu Seya, Papii Wamwangukia Rais Magufuli

MWANAMUZIKI Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ ambao wanasota jela kwa kosa la kuwanajisi watoto 9, wamedaiwa kusaka uwezekano wa kujinasua gerezani kwa kumuangukia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Taarifa kutoka kwa chanzo makini zimeeleza kuwa wanamuziki hao kwa kushirikiana na ndugu zao, wamemuandikia barua binafsi rais ili aweze kusikia kilio chao na ikiwezekana wasamehewe kutokana na mamlaka aliyo nayo.

“Si unakumbuka kipindi kile waliwahi kumuandikia waraka JK (Jakaya Kikwete, rais wa awamu ya nne) kumuomba awasamehe lakini bahati mbaya maombi yao hayakuzaa matunda! Wameona wajaribu kwa Magufuli ili ikiwezekana kupitia ile sheria inayompa mamlaka rais kusamehe mtu yeyote aliyehukumiwa kwa kosa lolote, awasamehe kina Babu Seya,

“Nasikia wameshaandika barua, wanaipeleka ikulu na wana imani Magufuli ni mtu anayeguswa sana na hofu ya Mungu, huenda akawasamehe,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa mtoto mkubwa wa Babu Seya, Mbangu Nguza na kuulizwa kama wamepeleka barua hiyo na matumaini ya ndugu zake kutoka gerezani, hakutaka kukubali au kukataa lakini akasema wao wana imani muda wowote ndugu zao watatoka gerezani.

“Kila siku nimekuwa nikisisitiza hili suala, labda niseme tena, Babu Seya na Papii watatoka siku si nyingi kutoka sasa,” alisema Mbangu.

Amani liliwasiliana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa na kumuuliza kama wamepokea barua hiyo, alisema hawajaipata na kuomba apewe muda afuatilie na atatoa majibu.

“Sijaiona hiyo barua, ngoja nitafuatilia na nitakujulisha,” alisema Msigwa.

KUMBUKUMBU

Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanaye watatu, Papii Kocha, Mbangu na Francis.

Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu hiyo.

Wakili wao, Mabere Nyaucho Marando akapeleka suala hilo Mahakama ya Rufaa Tanzania ambako Mbangu na Francis waliachiwa huru, Babu Seya na Papii wakaonekana bado wana hatia.

Babu Seya na wanaye walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka na kulawiti watoto hao kati ya Aprili na Oktoba, 2003 katika maeneo ya Sinza ya Palestina, Dar es Salaam. Mpaka sasa wana miaka 12 gerezani.

Chanzo:GPL

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHACHANDU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top