NI mateso. Ndivyo unavyoweza kusema, hasa baada ya kundi la maharamia
linalojishughulisha na bishara ya ‘unga’ nchini Pakistan kuelezwa
kumtesa kijana Mtanzania, Adamu Akida.
Kutokana na hali hiyo, timu ya MTANZANIA ilipiga kambi jana katika eneo
la Magomeni, Mtaa wa Idrissa, ambako pamoja na mambo mengine,
ilifanikiwa kuzungumza na kaka wa Adamu aliyejitambulisha kwa jina la
Hemed Abdallah (si jina lake halisi).
Akisimulia mkasa huo, alisema miezi minane iliyopita, Adamu alikwenda
kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina
la Juma, na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa
ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.
Baada ya kueleza shida yake hiyo, kaka yake huyo (Juma) alimuhoji kama
yupo tayari kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi, na Adamu alikubali
kufanya kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata pesa.
“Adamu kwa sasa ameshikiliwa kwa muda wa miezi minane, hatujui kama
alikuwa ameingia katika janga hili hadi pale tulipoona video zake katika
mitandao ya kijamii. Hapa aliyepo ni baba yake mdogo, Kessy Baharia na
baba yake mzazi yupo Bagamoyo Mlingotini, ndiko anakoendelea na maisha
yake.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma na
kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya hali
hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa
wameambatana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye jina
lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa
Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku
tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo
Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko ana angerudi mwezi
wa tisa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui kama
tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa
tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi sana
hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia magari,”
alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.
Mke wake
Inaelezwa kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.
Kwamba alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.
“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa Adamu anajua
kinachoendelea, maana miezi mitatu iliyopita alihama Magomeni na kuhamia
Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu anarejea nchini.
“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa hata kupatikana
hapatikani, na hatujui amehamia nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema
Abdallah.
Serikali ya Mtaa
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Srikali ya Mtaa wa Idrissa, Issa
Mpangile, alisema kuwa jana askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika
nyumba ya baba mdogo wa Adamu.
Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia, ambaye ndiye baba mdogo
wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye wakarudi katika
ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo ya mwenyekiti huyo.
Akizungumza kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa
huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa
Idrissa, Kata ya Magomeni.
Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Wakati Adamu anahama Mtaa wa Idrissa, alikuwa bado ni kinyozi na hakuna
rekodi kwamba alikuwa anasafiri nje ya nchi,” alisema Mpangile.
Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.
Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo
anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba
atakwenda kuripoti kituo cha polisi.
Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kuhoji
kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.
Serikali yahaha
Baada ya taarifa hizo kuripotiwa na gazeti hili jana, Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi wanafanya mawasiliano na Serikali
ya Pakistan ili kuangalia namna ya kumwokoa Adamu katika mikono ya
maharamia hao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba, alisema tayari wamepata taarifa dhidi ya Mtanzania huyo.
“Kwa sasa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa Pakistan tuone namna ya
kumtoa kijana huyo katika mikono ya hao watekaji, na tukikamilisha hilo
tutatoa taarifa rasmi juu ya jambo hili,” alisema Advera.
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kupitia mmoja wa maofisa wa idara ya
habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema wamepata
taarifa ya tukio hilo, na sasa wanafanya mawasiliano na Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi.
Source: Mtanzania